Pages

Naibu Kadhi Mkuu, Sheikh Abubakar Zuber Aonya Imani za Kishirikina

Waislamu nchini wametakiwa kujiepusha na imani za kishirikina kwani kwa kufanya hivyo ni kuidhalilisha dini hiyo.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Kadhi Mkuu, Sheikh Abubakar Zuber katika Maulid ya Mtume (S.A.W) iliyoandaliwa na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi, Dk Najim Msenga mwishoni mwa wiki katika Halmashauri ya Bumbuli, wilayani Lushoto mkoani Tanga.

Sheikh Zubeir, ambaye pia ni Naibu Mufti wa Tanzania, alisema viongozi wa dini hiyo na mashehe kukubali kudhalilishwa na waganga wa kienyeji maarufu kwa jina la Lambalamba ni kufedhehesha uislamu na kuwataka waepuke vitendo hivyo ili kuutukuza Uislamu.

Eneo hilo la Bumbuli miezi miwili iliyopita lilikumbwa na wimbi la vurugu zilizosababishwa na kukamatwa kwa watu 32 kutokana uchochezi uliotokana na waganga hao wa Lambalamba.

Watu hao walikamatwa Aprili 21 mwaka huu Bumbuli na kusababisha wananchi kufanya vurugu iliyopelekea kuchomwa kwa kituo cha Polisi, ofisi ya Afisa Tarafa pamoja na ofisi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo .

Sheikh Zubeir aliiitaka Serikali kuchukua hatua kali dhidi ya watu kama hao ambao nia yao ni kufanya vitendo vya kuondoa kuaminiana miongoni mwa Watanzania .

Alisisitiza juu ya umuhimu wa kulinda amani iliyopo bila kubaguana kwa misingi ya dini wala rangi, ili kuendeleza umoja uliopo baina ya watanzania.

Alisema ili nchi iwe na amani, lazima vitendo viovu vidhibitiwe na kuitaka Serikali kupiga marufuku kabisa vitendo hivyo.

Alimtaka Mbunge wa Bumbuli, January Makamba kusaidia katika kudhibiti waganga hao haramu ili kulinda heshima ya Bumbuli.
‘‘Ndugu waumini wenzangu, kwa pamoja sote tuhakikishe tunailinda amani iliopo kwa gharama yoyote, kwani panapo amani kila kitu kinaweza kufanyika.’’