Pages

Majanga Yamkuta Anaemiliki Home Shopping Center, Amwagiwa Tindikali

TindikaliMFANYABIASHARA maarufu na Mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center (HSC), Said Mohamed Saad, amemwagiwa tindikali maeneo ya Msasani City Mall, jijini Dar es Salaam juzi, muda wa saa moja jioni akiwa dukani kwake. Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha MTANZANIA Jumapili, mhusika wa tukio hilo mara baada ya kukamilisha azma yake, alikimbia, lakini mlinzi wa eneo hilo alijaribu kumkimbiza pasipo mafanikio, baada ya kuteleza na kuanguka.
Alisema hatua hiyo ilitoa mwanya kwa mtuhumiwa kutoroka eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki.
Taarifa ambazo pia zipo katika mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa Saad ambaye amelazwa katika Hospitali ya Trauma (AMI) iliyopo Msasani jijini Dar es Salaam, amepata madhara katika macho yake mawili, huku moja likiwa limeumizwa zaidi.

Aidha taarifa zaidi zinasema kuwa Saad anaweza kuzungumza, japo amefungwa mashine sehemu ya pua kwa ajili ya kumsaidia kupumua, huku madaktari wakiendelea kumhudumia hospitalini hapo.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, ambaye alisema kuwa yuko nje ya mkoa wa Dar es Salaam, na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na msaidizi wake.

Gazeti hili lilimtafuta Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Yusuph Mrefu, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Kamanda Mrefu alisema mpaka wakati anazungumza na gazeti hili, Saad alikuwa amelazwa hospitalini akiendelea na matibabu.

Mrefu alishindwa kuweka wazi majeraha aliyoyapata muathirika huyo wa tindikali, kwa madai kuwa bado hajamuona, lakini jitihada za Jeshi hilo zinafanyika ili kumkamata mhusika.

Akisimulia kuhusu tukio hilo, Kamanda huyo alisema Saad alikuwa dukani kwake maeneo ya Msasani akiongea na mfanyakazi wake, ghafla alitokea kijana ambaye alimmwagia kitu chenye maji usoni.


“Wahusika bado tunawasaka, si tukio la kumkamata mtu mara moja, kwani lilikuwa la ghafla, ilitokea saa moja jioni …hawakuweza kumbaini kwani alitokomea wakati wao wakimkimbiza mwathirika kituo cha polisi ili awahishwe hospitali,” alisema Kamanda Mrefu.

Mbali na kumiliki maduka hayo, Saad anatajwa kuwa wakala wa kuingiza makontena ya mizigo kwa ushuru mdogo toka nchini China.

Taarifa zilizozagaa katika mitandao ya kijamii zinasema kuwa mmiliki huyo wa HSC aliweka kambi Dodoma wakati wa Bunge la Bajeti na kuwahonga wabunge mamilioni ya shilingi ili wasijadili jambo hilo bungeni.

Inadaiwa kuwa mmliki huyo wa Home Shopping Centre amekuwa akipitisha zaidi ya makonteina 200 kwa siku bila kulipa kodi kwa zaidi ya miaka sita bila serikali kuchukua hatua.

Suala hilo ambalo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara, lilizua mjadala wakati fulani, na kusababisha baadhi ya watu waanze kuhoji uhusiano wake na serikali iliyoko madarakani.
  Na AGATHA CHARLES