Pages

Pata Kusoma Wasifu wa Wagombea Urais wa Kenya

Wycliffe Musalia Mudavadi, Martha Wangari Karua, Peter Kenneth, Mohammed Abduba Dida, Paul Kibugi Muite, Raila Amollo Odinga, Uhuru Muigai Kenyatta, na James ole Kiyiapi Kwa kuwa uchaguzi wa Kenya umepangwa kufanyika tarehe 4 Machi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imetangaza wagombea wanane watakaoshindania nafasi hizo za juu za nchi. Ufuatao ni wasifu wa kila mgombea wa urais, wamepangwa kialfabeti.

Kutoka juu kushoto, kuelekea mbele: Wycliffe Musalia Mudavadi, Martha Wangari Karua, Peter Kenneth, Mohammed Abduba Dida, Paul Kibugi Muite, Raila Amollo Odinga, Uhuru Muigai Kenyatta, na James ole Kiyiapi.
Mohammed Abduba Dida. [Jalada]
Martha Wangari Karua. [Tony Karumba/AFP]
Peter Kenneth. [Jalada]
Uhuru Muigai Kenyatta. [Simon Maina/AFP]
James ole Kiyiapi. [Tony Karumba/AFP]
Wycliffe Musalia Mudavadi. [Jalada]
Paul Kibugi Muite. [Jalada]
Raila Amollo Odinga. [Will Boase/AFP]

Mohammed Abduba Dida alizaliwa mwaka 1975 katika wilaya ya Wajir. Dida, aliyekuwa mwalimu, anagombea urais kupitia Muungano kwa ajili ya Mabadiliko Halisi (Alliance for Real Change). Mgombea mweza wake ni Joshua Odongo Onono, pia alikuwa mwalimu.
Dida, mpya katika siasa, ameapa kuwa Rais ambaye ataawangalia maskini. Alisema elimu inapaswa kuwa bure kwa Wakenya wote, na siyo kwa kutegemea mfumo wa ruzuku. Dida ameelezea kwa kujiamini kwa uwezo wake wa..
kufanya vizuri katika uchaguzi, kama alivyosema chama chake kinaungwa mkono sana na vijana.
Ana digrii ya elimu kutoka chuo kikuu cha Kenyatta na kwa sasa anafanya digrii ya uzamili katika masomo ya dini kutoka chuo kikuu cha Nairobi.
Dida amefundisha katika shule kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufundisha fasihi ya Kiingereza na dini katika shule ya sekondari ya Daadab katika kambi mchanganyiko ya wakimbizi na baadaye katika shule ya Lenana.
Alijiuzulu kufundisha mwaka 2009 na kuanza kazi ya uwakala wa kazi ya muda, lakini alisema mradi haukufanikiwa kwa sababu ya rushwa ya serikali.

Martha Wangari Karua Martha Karua, mgombea pekee mwanamke, katika kinyang'anyiro cha urais, alizaliwa Septemba 1957 huko Kirinyaga, Jimbo la Kati. Karua, mbunge wa Gichugu, anagombea kupitia National Rainbow Coalition pamoja na aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Bunge la Afrika Mashariki Augustine Lotodo.
Karua ameapa kuwakilisha muungano wa Kenya pamoja na jukwaa la mabadiliko ya uchumi na jamii, ikiwa ni pamoja na huduma za afya kila mahali na kuifanya Kenya kuwa kitovu cha uchumi katika kanda. Alisema atatoa asilimia 10 ya bajeti ya Kenya kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuongeza vyanzo vya nishati rejezi na kufanya kazi kuwa ili kuwezesha ufikivu wa intaneti kwa asilimia 50 kwa Wakenya katika miaka mitano.
Wakati wa mjadala wa urais, alisema atashughulikia kima cha juu cha vifo vinavyotokana na uzazi kwa kutoa upatikanaji wa huduma za afya mahali kote.
Karua ana digrii ya sheria kutoka chuo kikuu cha Nairobi na digrii ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani, Nairobi.
Kuanzia mwaka 1981 hadi 1987, Karua alifanya kazi mahakamani, alipanda kutoka hakimu wa wilaya hadi hakimu mkuu mkazi. Baada ya hapo amekuwa na shirika la uwakili binafsi hadi 2002.
Mwaka 1992, Karua alichaguliwa kuwa mbunge wa Gichugu, kiti ambacho anakishikilia hadi sasa.
Mwaka 1997 na 1998, alifanya kazi na kikundi cha Bunge cha Vyama Mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nchini Kenya. Mwaka 2008, Karua aliteuliwa kuwa waziri wa sheria, mshikamano wa taifa na masuala ya katiba akifanya kazi kama waziri wa usimamizi na maendeleo ya rasilimali za maji.
Mwaka 2009, Karua alijiuzulu katika nafasi yake ya uwaziri katika serikali ya umoja akitaja kukatishwa tamaa katika kutekeleza kazi zake.

Peter Kenneth Peter Kenneth alizaliwa Novemba 1965 huko Bahati, Nairobi. Yeye ni mbunge mwenye taaluma ya masuala ya benki. Anagombea urais chini ya chama cha Kenya National Congress, pamoja na mgombea mwenza Ronald Osumba, aliyekuwa meneja mwandamizi wa Safaricom.
Kama mgombea, Kenneth amejielekeza katika kuboresha tatizo la ukosefu wa ajira na uhakika wa chakula. Pia alidhamiria kuipa polisi vifaa na kuwalipa vizuri maofisa ili kuwahamasisha kufanya kazi nzuri, na anaamini kwamba maendeleo na elimu katika maeneo yanayokumbwa na uhalifu yatazuia vitendo haramu. Anapanga kulipia programu zake kwa kupunguza matumizi makubwa ya serikali.
Kenneth ana shahada ya kwanza na ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, pamoja na kozi ya shahada ya juu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Programu ya Utendaji kwa ajili ya Maendeleo ya Usimamizi huko Lausanne, Uswizi.
Kama mkurugenzi wa benki, Kenneth alianza kufanya kazi na Kampuni ya Fedha ya Nationwide mwaka 1985, kisha akafanya kazi na Prudential Finance na Benki tangu 1986 hadi 1997, ambako alikuwa meneja. Kuanzia 1997 hadi 2002, alifanya kazi katika Kampuni ya Kukata Bima ya Kenya, wakati huo huo akishika vyeo katika Shirika la Kukata Bima la Afrika na Benki ya Maendeleo ya Viwanda. Tangu 1998 hadi 2009, alifanya kazi kama mwenyekiti wa Kampuni ya Kukata Bima ya Zep.
Katika maisha yake ya kisiasa, Kenneth alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge wa kiti cha Gatanga mwaka 2002, kiti anachokishikilia hadi sasa.
Tangu 2003 hadi 2005, alifanya kazi kama msaidizi wa waziri katika Wizara ya Maendeleo ya Ushirika na Masoko, kisha kama msaidizi wa waziri katika Wizara ya Fedha hadi 2007. Tangu 2008, amekuwa msaidizi wa waziri katika Wizara ya Mipango, Maendeleo ya Taifa na Dira ya 2030.

Uhuru Muigai Kenyatta Uhuru Muigai Kenyatta alizaliwa Oktoba 1961. Baba yake ni rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, ambaye aliongoza tangu 1964 hadi 1978. Ni mgombea wa urais wa chama cha Jubilee Alliance, chama cha muungano kilichoundwa chini ya The National Alliance cha Kenyata na chama cha United Republican cha William Ruto.
Katika ilani ya muungano wake, Kenyatta ana msimamo wa Kenya iliyoungana "chini ya ndoto moja ya kujenga Kenya bora". Alisema atajikita katika suala la umiliki wa ardhi, na anadhamiria kuibadili Kenya kuwa kitovu cha uchumi, akijenga uchumi wa usafirishaji bidhaa nchi za nje.
Kenyatta ana shahada ya kwanza katika siasa na uchumi kutoka Chuo cha Amherst huko Marekani.
Baada ya kipindi kifupi cha kufanya biashara, Kenyatta aligombea kiti cha ubunge cha Gatundu Kusini mwaka 1997, lakini alishindwa. Miaka miwili baadaye, Rais Daniel arap Moi alimteua kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Kenya, na mwaka 2001, alimteua bungeni.
Kenyatta aligombea urais bila ya mafanikio mwaka 2002, lakini alishinda kiti cha ubunge akiwakilisha Gatundu kusini mwaka huohuo.
Aligombea urais tena mwaka 2007, lakini alijitoa na kumuunga mkono Rais Mwai Kibaki kwa uchaguzi wake tena. Kibaki alimteua Kenyatta waziri wa serikali za mitaa mwezi Januari 2008 kabla ya kuwa naibu waziri mkuu na waziri wa biashara mwezi Aprili 2008 kama sehemu ya serikali ya umoja iliyopanga kumaliza vurugu baada ya uchaguzi 2007.
Alihamishiwa katika Wizara ya Fedha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, wakati akiendelea kuwa naibu waziri mkuu. Aliacha kazi ya uwaziri wa fedha mwezi Januari 2012 baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kumtuhumu kwa kufanya uhalifu kinyume cha ubinadamu kwa wajibu wake katika vurugu za uchaguzi wa 2007-2008.
Wote Kenyatta na Ruto walikabiliwa na upinzani wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusiana na kesi zao zilizosimamishwa na ICC, na Kenyatta alijibu maswali kuhusiana na suala hili wakati wa mdahalo wa urais.

James ole Kiyiapi James ole Kiyiapi alizaliwa mwezi Mei 1961 huko Osupuko, Jimbo la Bonde la Ufa. Katibu Mkuu wa zamani katika wizara mbalimbali, aliacha kazi mwaka 2012 ili kugombania pamoja na mwanamke mfanya biashara Winnie Kaburu chini ya Urejeshaji na Kukijenga chama cha Kenya Party.
Kiyiapi anasimamia ilani ya uchaguzi inayokana siasa za kikabila. Alisema kipaumbele chake cha awali kitakuwa kuzingatia ukosefu wa ajira kwa vijana, ambalo aliita janga la taifa. Serikali yake, alisema, itashinikiza kazi ya kumaliza migogoro ya ardhi kwa uangalifu wa hali ya juu na uwazi, na itaboresha uzalishaji wa kilimo nchini.
Kiyiapi ana shahada ya uzamili kutoka katika Chuo Kikuu cha Moi na shahada ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Kanada, zote ni kuhusu misitu.
Kuanzia mwaka 1988 hadi 1994, alikuwa mtafiti mwandamizi katika kitivo cha Utafiti wa Mazingira katika Chuo Kikuu cha York nchini Kanada. Alifanya kazi kama mhadhiri na Profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Moi kuanzia mwaka 1994 hadi 2006.
Wakati huo, pia alifanya kazi kama mkurugenzi wa programu nchini katika Mfuko wa Wanyamapori Afrika.
Kiyiapi aliteuliwa kuwa katibu mkuu katika Wizara ya Mazingira na Maliasili mwaka 2006, Wizara ya Huduma za Tiba mwaka 2008, na Wizara ya Elimu mwaka 2010.

Wycliffe Musalia Mudavadi Naibu Wairi Mkuu Wycliffe Musalia Mudavadi alizaliwa mwezi Septemba 1960 huko Sabatia, Jimbo la Magharibi. Anagombea kupitia chama cha United Democratic Forum katika Amani Alliance, pamoja na Jeremiah Kioni, mbunge kutoka Jimbo la uchaguzi la Ndaragwa.
Mudavadi ameahidi kukuza uchumi wa uhakika nchini Kenya kwa kuzingatia utawala bora na kupunguza umaskini. Alisema atakabiliana na rushwa nchini kwa kupanga upya mfumo wa mahakama, na kuajiri maofisa polisi wengine zaidi ili kuboresha usalama.
Mudavadi ana shahada ya uchumi wa ardhi kutoka katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Baada ya kuhitimu, alifanya kazi katika Shirika la Nyumba la Taifa kabla ya kufanya kazi katika kampuni ya Tysons Limited inayohusika na ujenzi na upangishaji wa nyumba.
Mudavadi alikuwa mbunge mwaka 1989, wakati alipochaguliwa bila kupingwa kuchukua kiti cha ubunge wa Sabatia kilichoachwa wazi baada ya kifo cha baba yake, Moses Mudavadi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, Mudavadi aliteuliwa kuwa waziri wa fedha kwa miaka mitano. Mwaka 1998, aliteuliwa kuwa waziri wa kilimo, kisha waziri wa habari, uchukuzi na mawasiliano mwaka 1999, na waziri wa uchukuzi na mawasilino mwaka 2001. Kwa kipindi chote hiki alishikilia kiti cha ubunge wa Sabatia.
Mwaka 2002, Mudavadi alipoteza kiti chake cha ubunge, lakini aliteuliwa na Rais Daniel arap Moi kuwa makamu wa rais na alishikilia nafasi hiyo kwa miezi miwili. Kisha aligombea bila mafanikio nafasi ya makamu wa rais na mgombea mwenza Uhuru Kenyatta mwaka 2002.
Baada ya hapo, Mudavadi alisaidia kuanzisha chama cha Orange Democratic Movement na aligombea kwa nafasi ya rais wa chama mwaka 2007, lakini Raila Odinga alimshinda.
Tangu hapo, alikuwa akifanya kazi kama mjumbe wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Dunia na mjumbe wa Kamati ya Bunge iliyochaguliwa kwa ajili ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwaka 2012, Mudavadi aliondoka katika chama cha Orange Democratic Movement na kujiunga na chama cha United Democratic Front. Kwa muda mfupi alijiunga na chama cha Jubilee Alliance cha Uhuru Kenyatta, lakini aliamua kujitenga mwezi Desemba baada ya kutokubaliana kuhusu nani atakayeongoza.

Paul Kibugi Muite Paul Kibugi Muite alizaliwa mwezi wa Aprili 1945. Ni mbunge wa zamani kutoka Kabete ambaye ni mwanachama muanzilishi na kiongozi wa Chama cha Safina. Anagombea pamoja na Shem Ochuodho, waziri wa zamani wa nishati na mbunge kutoka Rangwe.
Muite alisema, yeye kama rais atashughulikia ukosefu wa ajira na kuboresha hali za kazi, sehemu moja kwa kupandisha mishahara na kuimarisha sheria za kazi ambazo zinaweka kikomo cha saa siku ya kazi kuwa masaa manane. Pia aliapa kuzuia ufisadi wa serikali, jambo alilosema kuwa "limewapeleka mamilioni ya Wakenya katika umasikini wa milele na mateso".
Anasema anaamini kwa umoja wa Wakenya wote, bila ya kujali makabila yao, na atafanyia kazi uboreshaji jamii na uchumi kwa watu wote. Muite anasema Kenya pia inaumizwa na sifa hasi kimataifa kwa ufisadi na rekodi mbaya ya haki za binadamu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia kupitia elimu na masoko.
Muite, mwanasheria wa haki za binadamu, alikuwa mtu maarufu wakati wa siku za mwisho za mfumo wa chama kimoja miaka ya 1990, ambayo ilianzishwa na Kenya African National Union (Chama cha Kitaifa cha Waafrika wa Kenya) mwaka 1982.
Alitumikia vipindi vitatu vya miaka mitano mitano kama mbunge wa Kabete, mwaka 1992, 1997 na 2002.

Raila Amollo Odinga Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga alizaliwa tarehe 7 Januari mwaka 1945 huko Maseno Jimbo la Nyanza, mtoto wa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga. Anagombea katika chama cha Orange Democratic Movement (Harakati Kidemokrasia za Chungwa) pamoja na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kama mgombea wake mwenza.
Odinga amejikita katika vijana kwenye kampeni zake, akiwaahidi kupata ajira na elimu. Alisema kuwa atatoa pesa taslimu kwa masikini na wazee, na kuanzisha mpango kwa vijana wanaosubiri kuingia chuo kikuu au wanaotafuta kazi kwa kufundisha kwenye shule za msingi.
Kiuchumi, alisema ataanzisha progamu za kusafirisha bidhaa zinazotengenezwa vijijini nchini Kenya, na kusaidia ukuaji wa sekta ya chuma cha pua. Alisema kuwa ataboresha miundombinu na kupanua uwekezaji katika usalama wa chakula kupitia kilimo kilichoboreshwa, ruzuku kwa wakulima na utafiti.
Odinga anayo shahada ya uzamili ya uhandisi mitambo kutoka Chuo cha Magdeburg Cha Tekonolojia ya Juu. Pia ametunukiwa digirii za heshima za uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida huko Tallahassee, Marekani.
In 1970, alianza kufanyakazi kama mhadhiri kwenye idara uhandisi mtambo katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Mwaka 1974, aliondoka wakati alipoteuliwa kama meneja wa viwango katika kikundi kwenye Ofisi mpya ya Viwango ya Kenya, ambako alikuwa naibu Mkurugenzi mwaka 1978.
Mwaka 1982, Oginga Odinga alihusishwa kama mtoa fedha wa jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Raisi Daniel arap Moi, ambaye alikuwa amezuwia jaribio la Oginga Odinga la kusajili chama cha upinzani. Raila Odinga alishitakiwa kwa uhaini na kuwekwa kuzuizini kwa muda wa miaka sita bila kesi.
Odinga aliachiwa huru mwaka1988, lakini na kutiwa mbaroni tena mwaka mmoja baadaye kwa kuhusika na Harakati za Mapinduzi Kenya, kikundi kilichokuwa kkinashinikiza kuwepo kwa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya.
Odinga alikamatwa tena mwaka 1990 na alipoachiwa huru mwaka 1991 aliomba hifadhi huko Norway, kwa madai kwamba serikali ilikuwa inapanga kumuua.
Baadya ya mwisho wa mfumo wa chama kimoja, Odinga alirejea mwaka 1992 na kujiunga na Jukwaa la Demokrasia (FORD), chama cha siasa kilichokuwa kinaongozwa na baba yake, na kushinda kiti cha ubunge katika eneo la ubunge la Langata.
Mwaka wa 1997, Odinga alishindwa alipogombania urais.
Odinga alifanyakazi kama waziri wa nishati kutoka mwaka 2001 hadi 2002 na kama waziri wa barabara, kazi za umma na nyumba kutoka mwaka 2003 hadi mwaka 2005.
Mwaka 2005, Odinga alianzisha chama cha Harakati za Kidemokrasia cha Chungwa, ambapo kwa kupitia chama hicho, aligombea uraisi bila mafanikio mwaka 2007. Baada ya kumalizika kwa vurugu, Odinga akawa waziri mkuu katika makubaliano ya kugawana madaraka.

CHANZO;sabahionline