Ndugu zangu, Tarehe kama ya leo miaka 20 iliyopita, yaani tarehe 2 Julai, 1992,
Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya kuruhusu
kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi.
Miaka 20 imetimu, tumepiga hatua, lakini, mpaka hii leo, bado upinzani
kwa wengine unatafsiriwa kama ni uadui, na wakati mwingine ni.. uhaini.
Na katika Tanzania yetu, wenye fikra za kukipinga Chama tawala, CCM na
Serikali wamekuwa wakitengwa na hata kupewa majina mabaya. Nimeshawahi
kumsikia mtu akiambiwa;
“Alaa, unaongea na Lipinzani hilo!” Kana kwamba aliyeitwa ‘ Lipinzani’ hakuwa Mtanzania na binadamu kama wengine.
Na hakika, katika kujadili hili la Katiba Mpya, tuna kila sababu ya
kuipitia historia yetu. Maana, naamini, kuwa historia ni mwalimu mzuri.
Itakumbukwa, katikati ya vuguvugu lile la mageuzi ya kisiasa miaka ya
90 mwanzoni, Watanzania zikatufikia habari; kuwa Oscar Kambona,
aliyekosana na Nyerere na aliyekimbila uhamishoni Uingereza, alikuwa
njiani kurudi nyumbani. Ujio wa Oscar Kambona ukawa gumzo la mjini na
nje ya jiji. Kuna waliojiandaa kwenda uwanjani kumpokea.
Usiku mmoja ikasikika sauti ya Bw. Mrema redioni. Sauti ya Waziri wa
Mambo ya Ndani. Mrema alitamka, kuwa kama Kambona angekanyaga mguu wake
Dar es Salaam, basi, angekamatwa kujibu mashtaka ya uhaini.
Ni hofu ile ile ya Serikali hata wakati huo. Hofu ya kuimarika kwa fikra
za upinzani na kukua kwa upinzani. Mrema akatumika au akajituma
kuwatisha na kuwakatisha tamaa Watanzania. Kambona alikanyaga Dar,
hakuwa na mashtaka ya kujibu. Ulikuwa ’ mkwara’ tu, kama wanavyosema
mitaani.
Na Mrema, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, aliifanya kweli kazi ya kuwa ’
Mbwa wa Serikali’. Alibwaka kweli kweli. Nakumbuka usiku mmoja mwanzoni
mwa miaka ya tisini nilimsikia Mrema akiongea redioni kutishia
maandamano ya CUF. Maandamano yale yalikuwa yahitimishwe kwa mkutano
viwanja vya Mnazi Mmoja. Mwenyekiti wa CUF, Bw. James Mapalala ndiye
alikuwa aongoze maandamano hayo na kuhutubia.
Augustino Lyatonga Mrema akaaunguruma redioni usiku ule. Alishusha ’
mkwara’ mzito. Kuwa maandamano hayo si halali na yangekutana na nguvu za
dola. Kesho yake, CUF waliingia mitaani. Ndio, Ungangari wa CUF ulianza
siku nyingi.
Pale Mnazi mmoja FFU wakamwagwa, na farasi wao pia. Virungu vilitembea.
James Mapalala, Mwenyekiti wa CUF, hakuonekana. Kukawa na taarifa, kuwa
anatafutwa na polisi.
Dar ilikuwa ndogo wakati huo, lakini James Mapalala hakupatikana .
Ninazo taarifa za kuaminika za Kibalozi, kuwa James Mapalala alikuwa amejificha kwenye moja ya makazi ya rafiki yake, balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Ni balozi gani huyo? Na nini hasa kilitokea miaka 20 iliyopita?
Ninazo taarifa za kuaminika za Kibalozi, kuwa James Mapalala alikuwa amejificha kwenye moja ya makazi ya rafiki yake, balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Ni balozi gani huyo? Na nini hasa kilitokea miaka 20 iliyopita?
James Mapalala yungali hai. Huu ni wakati kwa waandishi vijana
kuwatafuta wazee veterani wa harakati za mageuzi ya kisiasa hapa nchini.
Wazee kama akina James Mapalala.
Hawa ni watu muhimu sana watakaotusaidia kupokea simulizi zao. Kisha
ziwekwe kwenye maandishi, na iwe kumbukumbu za kihistoria. Ni historia
yetu, tusiionee aibu. Ni urithi tutakaowaachia wajukuu zetu ili nao
waweze kujifunza. Waweze kujitambua na kujenga mioyo ya uzalendo.
KiliNyepesi
No comments:
Post a Comment