Msaada wa kijeshi kwa Misri ungesitishwa endapo Marekani ingelitaja matukio ya wiki jana kama mapinduzi ya kijeshi. Kundi la Muslim Brotherhood linalomuunga mkono Morsi linasisitiza arejeshwe madarakani.
Wafuasi wake wamekua wakiandamana karibu na kambi kuu ya jeshi ambapo anaaminika kuuzuiliwa. Hapo Jumatatu,wafuasi wa Brotherhood 51 waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi wakati wanakabiliano.
Utawala wa mpito umesema kwamba Bw. Morsi anazuiliwa eneo salama na kwamba haki zake zinazingatiwa. Maafisa wa Marekani wamesema ndege mpya za kivita aina ya F-16 zitawasilishwa katika wiki chache zijazo.
Mpango wa kufadhili jeshi ulianza kutekelezwa mapema mwaka huu na jeshi linatarajia kupokea ndege 20 za kivita. Msemaji wa ikulu ya Rais amesema Marekani haitabadilisha mpango wa kufadhili jeshi la Misri, japo inaendelea kutathmini kuhusu matukio ya kisiasa. Msaada wa kijeshi nchini Misri ambao hutolewa na Marekani hufikia dola bilioni 1.3 kila mwaka.
Hapo Jumanne, kibali cha kumkamata kiongozi wa Muslim Brotherhood Mohamed Badie kilitolewa pamoja na wakuu wengine tisa wa kundi hilo. Viongiozi hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia mjini Cairo ambapo zaidi ya watu 50 waliuawa na mamia kujeruhiwa.
BBC Swahili