WAKATI Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare akiwa nje kwa dhamana mwezi mmoja sasa, mwenzake Ludovick Joseph(mwenye pingu) anaendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisumu, wakati kesi inayomkabili Lwakatare na mwenzake ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana.
Wakili wa Serikali, Mkuu Ponsian Lukosi alidai mahakamani kwamba upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa na mshtakiwa Ludovick hajatimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Katemana alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 22 mwaka huu na aliamuru mshtakiwa aendelee kuwepo rumande hadi atakapopata wadhamini watakaotimiza masharti.
Lwakatare na Ludovick walikubaliwa dhamana baada ya kufutiwa mashitaka matatu ya ugaidi na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kubakiwa na shitaka moja la kula njama ya kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Katemana baada ya kupitia hoja za kuomba dhamana zilizotolewa na wakili Peter Kibatala, alikubali kuwapa dhamana washtakiwa hao kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wanaotoka katika taasisi zinazotambulika kisheria, ambao kila mmoja atasaini dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe.
Hakimu Katemana pia aliwataka washitakiwa hao kusalimisha hati zao za kusafiria mahakamani na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.
Juni 10 mwaka huu, baada ya kukubaliwa dhamana, Lwakatare alidhaminiwa na kumwacha Ludovick akiendelea kusota rumande kwa kukosa wadhamini.
Hata hivyo uamuzi wa kuwapa dhamana washtakiwa hao ulikatiwa rufaa na upande wa Jamhuri katika Mahakama Kuu ya Tanzania wakipinga hatua hiyo.
Pia Jamhuri iliwasilisha maombi katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ikitaka ifanyie marejeo uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kuyafuta mashtaka matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao. Uamuzi huo ulitolewa na Jaji Laurence Kaduri.
Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18, mwaka huu wakikabiliwa na mashitaka hayo manne ya ugaidi, ambayo baadaye yalifutwa na Hakimu Emilius Mchauru baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kudai hana nia ya kuendeleza mashitaka ya ugaidi dhidi yao.
Baada ya kufutiwa mashitaka hayo, washitakiwa hao walikamatwa tena na kufunguliwa mashitaka mengine yanayofanana na hayo mbele ya Hakimu Katemana ambayo pia yalifutwa na Jaji Kaduri.
NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MTANZANIA
MTANZANIA