Pages

MARUFUKU KUANDIKA KUHUSU MGOGORO WA CONGO-JWTZ

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),  limevitaka vyombo vya habari kuacha kuandika taarifa za mgogoro wa  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), badala yake taarifa rasmi  zitakuwa zikitolewa na jeshi hilo kila baada ya wiki mbili.

Katazo hilo limetolewa juzi jijini Dar  es Salaam na Meja Erick Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu maendeleo ya mgogoro huo.

Alisema hali hiyo inatokana na jeshi  hilo kubaini kuwa baadhi ya vyombo vya habari nchini vinaandika habari  za uchochezi zinazotaka kuziingiza vitani nchi ya Tanzania na Rwanda.(P.T)
                                         
Meja Komba alisema hategemei kama  kutakuwa na chombo chochote cha habari kitakachotoa habari kuhusu  maendeleo ya mgogoro huo bila kupata taarifa rasmi kutoka jeshi hilo.

Alionya kuwa chombo chochote kitakachokwenda kinyume kitakuwa kina tatizo.
Meja Komba alisema wananchi wanapaswa  kuelezwa kuwa kikosi cha Tanzania kilichoko DRC ni sehemu ya Brigedia ya  SADC, iliyotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa (Monusco).

Alitaja majukumu ya kikosi hicho kuwa  ni kuzuia waasi wa M23 na wengine kujitanua, kuvunja nguvu zao na  kuyapokonya silaha makundi yote ya waasi.
"Kwa kuzingatia kuwa kikosi chetu kiko  chini ya majeshi ya Monusco, inamaanisha kuwa operesheni hiyo ni ya  Umoja wa Mataifa," alisema.

Aliongeza kuwa Tanzania haikupeleka  kikosi chake DRC kwa ajili ya kupigana na M23, pia ieleweke kuwa haina  tatizo na Rwanda kuhusiana na operesheni hiyo ambapo Rwanda ilitoa  ridhaa kikosi cha Tanzania kwenda DRC.

Meja Komba alisema Rwanda ni miongoni  mwa wanachama wa nchi za Maziwa Makuu, ambayo imesaidia kwa kuruhusu  kikosi cha Tanzania kupitisha vifaa na zana katika nchi yake kupeleka  DRC.
"Tanzania inashiriki katika operesheni  hiyo ya ulinzi wa amani nchini DRC kutokana na mgogoro kati ya serikali  na waasi hususan kikundi cha M23," alisema.
Mgogoro huo ulianza Aprili mwaka jana,  ambapo kikundi cha M23 kilijitoa katika jeshi la serikali na kuanzisha  mapigano yaliyosababisha hali ya usalama nchini DRC kuwa mbaya.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo  ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe Benard, amesema kuwa  marais Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda wamemaliza tofauti  zilizokuwa zimejitokeza kati yao hivi karibuni.

Marais hao walikutana na kufanya kikao  cha faragha jijini Kampala nchini Uganda juzi baada ya mkutano wa  viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na baadaye kutoa taarifa kwa waandishi  wa habari.

Kuzorota kwa mahusiano kati ya  viongozi hao kulikuja kufuatia kauli ya Rais Kikwete ya kumtaka Rais  Kagame kukaa meza moja na vikundi vya waasi wa nchi yake vilivyo nchini  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ushauri ulioonekana kumkera Rais  Kagame.

Akizungumza na waandishi wa habari  jana jijini Dar es Salaam, Membe alisema marais hao walitumia mazungumzo  yao yaliyochukua muda wa saa moja kujadiliana na kueleweshana mambo  mbalimbali yaliyosababisha kutoelewana.

"Baada ya mkutano huo ambao uliwapa  fursa za kuchambua, kujadili na kurejesha mahusiano ya kihistoria kati  ya nchi hizi mbili, marais wetu walitoka na nyuso za furaha," alisema.
Moja ya maazimio ya kikao chao ni kuwa na vikao vingine kati ya Rwanda na Tanzania katika siku zijazo.
"Kwa kweli kikao kati ya Rais Kikwete  na Rais Kagame kimeondoa majungu yote, kimekata fitina, uongo na maneno  ya kuchombeza yaliyokuwa yakitawanywa na watu mbalimbali hapa nchini na  hata kule Kigali," alisema.

Mbali ya kikao hicho pia Rais Kikwete  alifanya kikao kingine cha faragha na Rais wa Uganda Yoweri Museveni  ambapo walipata muda wa kujadiliana kwa kina kuhusu mambo mbalimbali  kuhusu nchi zao na mambo ya migogoro katika nchi za Maziwa Makuu.

Akizungumzia yale yaliyokubaliwa  katika mkutano wa viongozi wa nchi za Maziwa Makuu, Membe alisema kuwa  mkutano huo kwanza ulimruhusu Rais Museveni aendelee kusuluhisha vita ya  serikali ya DRC na waasi.

Alisema kuwa viongozi hao walilaani  mashambulizi ya M23 yaliyojeruhi na kumuua Meja Mshindo wa Tanzania  aliyekuwa miongoni mwa askari walioko nchini Congo katika kusimamia  amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Tanzania Daima