Baba mzazi wa Muigizaji wa kike wa filami nchini maarufu kama
Lulu, ambaye anahusishwa na kifo cha marehemu Steven Charles Kanumba,
ameibuka na kueleza kushtushwa sana na taarifa za kifo hicho pamoja
na habari kuwa bintiye alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na muigizaji
huyo nguli na kuwa anahusika na kifo chake. Baba Lulu, ambaye
alijitambulisha kwa jina la Michael Edward Kimemeta(49) mzaliwa wa
Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro, kaiambia Globu ya Jamii leo huko
Moshi kuwa alimtambua Steven Kanumba kama mwalimu wa mtoto wake
Lulu,lakini hakuamini masikio yake baada ya kupata taarifa za kifo
hicho, huku bintiye, anayedaiwa alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na
marehemu, anahusika.Lulu alifikishwa mahakamani
jana April 11, 2012 akikabiriwa na mashtaka ya mauaji ya Marehemu
Steven Kanumba, ikiwa ni siku nne baada ya kifo cha msanii huyo.
Alisema kuwa Elizabeth ama Lulu alizaliwa tarehe April 17,1995 katika
hospitali ya..
Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, na kwamba
alimaliza elimu ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Midway
mwaka jana na kamba hivi sasa ana umri wa miaka 17. Bw Kimemeta
alisema kuwa ni vyema polisi kuwa makini katika uchunguzi wao kwa
kuzingatia kuwa tukio hilo limejenga chuki na uhasama baina ya Lulu na
ndugu, jamaa, marafiki na wapenzi wa marehemu Steven Kanumba. Alisema
kuwa kilichomshtusha zaidi ni taarifa za polisi kusema kuwa kulitokea
ugomvi kati ya Marehemu Steve Kanumba na Lulu,huku ikitajwa kuwa
walikuwa wapenzi.
“Hatukutegemea kama Marehemu
Kanumba angeweza kuwa na mahusiano ya kimapenzi na binti yetu; kwanza
ndiye tuliyekuwa tukimtegemea kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza na
kukikuza kipaji alichokuwa nacho Elizabeth”, alisema baba mtu.
“Ninaomba Wanasheria na wanaharakati wa haki za kibinadamu kuingilia
suala hili na kusaidia katika kupatikana kwa haki dhidi ya shtaka la
mauaji linalomkabili binti yangu Elizabeth na pia naomba swala hili
lisichukuliwe kishabiki ama kwa hisia bali haki ichukue mkondo
wake”alisema.
Alisisitiza kuwa jamii inatakiwa kutambua
mazingira ya tukio hilo,ambapo chanzo kinasemekana ni ugomvi
uliopelekea tafrani kwa Lulu kutuhumiwa kumsukuma Marehemu Kanumba kwa
kile kinachodaiwa kuwa ulikuwa wivu wa kimapepenzi na haiyumkini
hakukusidua kumuua hivyo yeye anashangaa bintiye kuhusishwa moja kwa
moja na mauaji. “Ushiriki wa mwanangu kuhusu mambo ya sanaa
nilikwishapata wasiwasi na mama yake mzazi alikuwa akiwasiliana na
Marehemu Kanumba enzi za uihai wake ambaye alikuwa anamhakikishia
usalama wa Lulu na kusema kuwa ataendele kubaki kama mwalimu…..lakini
leo nasikia alikuwa ni mpenzi - nilishtushwa” alisema Kimemeta. Baba
Lulu pia ameelezea kusikitishwa kwake kwa kushindwa kuhudhuria mazishi
marehemu Steven Kanumba kuhofia usalama wake, na kusema mazingira
yatakaporuhusu hata sita kufika nyumbani kwa marehemu Steven Kanumba na
kutoa pole. Bw Kimemeta amesema kuwa anaungana na Watanzania wote
kutoa pole kwa familia ya Marehemu Steven Kanumba na kutoa mkono wa pole
kwa msiba huo mkubwa ambao haukutarajiwa.Kasema kuwa
Kanumba alikuwa bado ni kijana mdogo aliyeonyesha umahiri kwenye sanaa
na kwamba amecha pengo kwa familia yake na Tanzania kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment