Pages

One on one: One The Incredible

Ujio wake kwenye gemu uliambatana na msisimuko. Ngoma za masikio ya vichwa vya Hip Hop Bongo zikaanza kuwambwa upya kujiandaa kupokea mitetemeko inayotoka kwenye koo la One. One The Incredible.
Wakati ana miaka kama sita hivi, kaka zake walikuwa wanakutana na wasanii kama kina SOS B, na wakongwe wengine kwenye gemu la Hip Hop Tanzania miaka ya 90, kupiga tizi na kubadilishana ujuzi. Sidhani walikuwa wanatambua kuwa wanatengeneza Muujiza utakaokuja kushangaza watu miaka 20 baadae. Na muhimu zaidi, kusimamia nguzo zilizosimamishwa na waliotangualia.
Leo hii One anajitambua na anatambulika kama Kijana mwenye Kipaji na Mzawa wa Tanzania.
http://vijana.fm/wp-content/uploads/2011/03/One_Harry.jpg
One anategemea kufyatua mzigo wa nyimbo 24 wiki ijayo utakaokwenda kwa jina la “Soga Za Mzawa”. Bahati nzuri, tulipata muda wa kulonga naye na kujenga mambo mawili matatu…
1. Niambie Moko wa Miujiza?
Shwari.
2. Kwanza kabisa, kwanini uliamua kujiita “One” au “One The Incredible” au “Moko wa Miujiza”? Jina ulilipata wapi?
One ni jina nililopewa na mentor wangu at the time, Lord’s Child aka L.C. Yeye aliamua kuniita hivyo kutokana na flow na uandishi wangu.
3. Kitu gani kilikusukuma kuingia kwenye gemu, au watu gani walikusukuma mpaka ukashtukia unaliweza gemu? 
Kikubwa hasa kilikuwa ni kaka zangu… R.I.P.  Wao ndio walinitambulisha kwa rap. Baadae ikaja kuwa interest yangu baada ya kugundua hicho ndicho kitu pekee ambacho kila mtu alikuwa akinipongeza kwa uwezo niliokuwa nao, vitu nilivyokuwa nafanya. Basi nikaamua..
kuhangaikia bila pingamizi.
4. Nadhani wengi wanakubali kuwa One ana flow kali, na hapa sizungumzii maneno tu, bali na mtiririko wa fikra au mawazo. Unajisikiaje kusikia maneno kama hayo?
Ni faraja kubwa kwa kweli. Kutoka enzi zile nafanya na marafiki zangu mpaka kufikia hapa, ni kitu ambacho ni kama ndoto. Kwa kuwa, nani angeweza kuamini kama mimi nitakuwa mmoja wa emcees wanaosikika tu… achilia mbali kukubalika? Hata mimi mwenyewe nisingekuamini kama ungenieleza miaka minne iliyopita.
Ni baraka kwa kweli.
5. Kitu kingine muhimu ambacho umeonesha ni kuwa ni mwandishi mzuri sana wa mashairi. Kuna mtu aliyekufundisha kukaza vina? Una ushauri gani kwa watu ambao wangependa kufuata nyayo zako?
Mimi naamini mwandishi mzuri ni yule anayekubali kujifunza kutoka kwa waliomtangulia… Kwa vile unavyovisikia, unakuwa unapata jinsi ya kuwasilisha kitu tofauti kutokana na jinsi unavyoguswa na yule unayemsikiliza, na kile anachokitoa kwako.
6. Vipi, umemaliza au bado unaendelea na shule? Umeweza kumudu muziki na shule kwa wakati mmoja?
Bado naendelea na elimu mzazi. Bado muda mrefu sana mpaka niseme nimemaliza masomo. Kuhusu kumudu yote kwa mpigo, siku hizi nafanya muziki hisia. Masomo kama kawa, ila mziki pale nitakapokuwa na hisia ya kuandika au kurekodi… nd’o najihusuha nao.
7. Twende kwenye kazi zako za sanaa — One Incredible, Pure Namba, YGB (Young Gifted and Black), nadhani kila wimbo ulikuwa na kitu fulani. Hebu tuambie ulitaka kuwaambia nini watu kwenye hizo nyimbo tatu?
 Kwa ujumla santuri yangu ya kwanza “Soga Za Mzawa” inanihusu mimi, mimi binafsi kama mimi, na mimi kama kijana Mtanzania  ambaye nahangaikia kesho yangu iwe njema hapa nyumbani. Ujumbe wangu mkubwa ni kwamba, ukiamini wewe binafsi unaweza kitu, hata dunia nzima ikatae, utafanikisha tu.
Ukimwongelea Mzawa wa Tanzania, asilia, ni mtu asiye na uwezo, asiye na lolote. Lakini huyu anaweza kufanikisha malengo yake kwa kujitegemea mwenyewe tu.
8. Na ule ubeti kwenye “Hisia“, unabeba hisia za kijana ambaye anajaribu kulinda familia iliyotelekezwa na baba. Huu mstari ulioelekezwa kwa baba “Kama wewe ni nyani, basi mi’ ni simba”… Maneno mazito hayo!
 Kwenye ule ubeti nimeongea kama kijana aneyeona misingi ya familia ikiyumba. Ila yeye kama mhusika wa familia hawezi fanya lolote kwa sababu hajajua tatizo hasa. Masuala ya wazazi kugombana wazazi yapo, na sababu mara nyingi ni moja… Kutokupangilia maisha, badala yake kuegemea upendo baina ya watu wawili tu. Wazazi wanapogundua hamna upendo ndani ya ndoa, wanashindwa kuwaeleza watoto [wao] matatizo yao bianfsi, matokeo yake kuvunja ule msingi mzima wa familia.
Ile mistari inaeleza kiasi gani sababu zisizo za msingi za kuvunjika kwa familia zinanikera kama mhusika.
9. Mstari ambao wengi bado hawajausikia “Siuzi kura kama Bonta” umekuletea changamoto za hapa na pale. Ukiacha uchezaji wa maneno, ulikuwa unataka hadhira ipate ujumbe gani?
Wazo zima la kuuza kura si suala la busara. Kioo cha jamii hakipaswi ku-motivate, au kuchochea vitu kama hivi kwa sababu vina madhara makubwa. Kwa hiyo, kwa uelewa wangu, mawazo yako binafsi ukiyaweka mbele ya jamii yanaweza yakatumika au yakatumiwa na watu wenye uelewa mdogo, hasa ikiwa wewe ni public figure, yaani kioo cha jamii. So, it was a positive comment to the negative minded…
10. “Soga Za Mzawa”… kwanza, kwa nini umeipa santuri yako ya kwanza jina hilo? Itakuwa na maudhui gani?
Soga kwa Kiswahili fasaha ni hadithi fupi fupi. Na Mzawa ni mzaliwa halisi wa mahala fulani. Soga za Mzawa ni hadithi fupi fupi za mzaliwa wa Tanzania na maisha yake.
Kama nilivyodokeza awali, “Soga Za Mzawa” inanihusu mimi kama kijana Mtanzania ambaye nahangaikia kesho yangu iwe njema. Na naamini nikiamini naweza kitu, basi nitafanikisha tu.
11. Tupe dondoo zaidi kuhusu album; nyimbo ngapi, unategemea itapokelewaje na mashabiki wako wanaoendelea kuongezeka kila kukicha?
Kwakweli sijajua itapokelewa vipi. Hilo naliacha mikononi mwa mashabiki… Nyimbo zitakuwa 24!
12. Kuna lolote ambalo ungependa kuwaambia mashabiki wako na wa Hip Hop ya Tanzania kwa ujumla? 
Tuwe Pamoja. Support Hip Hop!.
13. Kama kawaida yetu, tungependa utuambie Top 5 emcees, na sababu!
1. Fid Q. Ndiye MC pekee ambaye miaka nenda rudi amekuwa akiendelea kunishangaza… kwa kubakia Hip Hop.
2. Prof. Jay. Nimejifunza mengi kwenye ngoma za huyu mzazi zaidi ya nilivyojifunza shule.
3. Hasheem Dogo, nimependa sana jamaa uwasilishaji wake, na jinsi anavyochagua maudhui kwenye mashairi yake.
4. Maalim Nash,  huyu jamaa ni darasa. Inspiration. Najivunia kuwa mmoja wa MC aliyebahatika kufanya naye kazi. Naamini ni baraka kuwa mmoja wa MCs anayesikilizwa na Nash.
5. Nikki Mbishi. Yule jamaa ni freestyle beast milele. Hilo halitobadilika kwangu.
Shukrani za pekee kwa Moko kwa kutupa wasaa wa kubadilishana mawili matatu. Tunamtakia kila la heri kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mwisho wa mwanzo wa safari yake. Juni 11, 2012, mitaa itakuwa inasikiliza Soga kutoka kwa Mzawa. Tega sikio ujue sehemu za kwenda kujipatika nakala yako.
Vitendo Dhidi ya Maneno!
Source: TZ Hip Hop

No comments: